Wabunge wahimiza Uingereza kutoa misaada kwa masharti

Kamati ya bunge la Uingereza inayohusika na misaada ya kimataifa imeitaka nchi hiyo kuwekea masharti makali misaada ya maendeleo kwa mataifa yaliyokumbwa na mizozo kama vile Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kamati hiyo inasema kuwa Uingereza ambayo ni mfadhili mkubwa wa Rwanda inafaa kuishinikiza nchi hiyo kuruhusu uhuru zaidi wa kisiasa.

Hata hivyo kama anavyoarifu mwandishi wa BBC wa masuala ya maendeleo ya kimataifa Mark Doyle hatua ya kuweka masharti kabla ya kutolewa misaada ni swala nyeti.

Kuna hofu kuwa iwapo Uingereza itachukua hatua kama hii, Rais wa Rwanda Paul Kagame huenda akasitisha uhusiano wote na nchi hiyo kama alivyofanya na Ufaransa miaka kadhaa iliyopita.