Mwanasayansi wa nuklia auawa Tehran

Ripoti kutoka Iran zinasema mwanasayansi mmoja wa nuklia ameuawa kwenye shambulio la bomu katika mji mkuu wa nchi hiyo Tehran.

Shirika la habari la FARS, limesema mtu mmoja aliyekuwa akiendesha pikipiki aliweka bomu kwenye gari la mwanasayansi huyo Mostafa Ahmadi Roshan.

Roshan ni muadhiri wa chuo kikuu na pia anafanya kazi katika kiwanda cha kurutubishia madini ya uranium ya Natanz.

Shambulio hilo ni la nne dhidi ya wanasayansi wa nuklia nchini humo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Mashambulio mawili yaliyopita pia yalitekelezwa na watu waliokuwa wakiendesha pikipiki ambao waliweka mabomu katika magari ya wanasayansi hao.

Serikali ya Iran imelaumu maafisa wa ujasusi wa Marekani na Israeli kwa kuhusika na shambulio hilo.

Shambulio hilo linajiri huku kukiwa na uhasama kati ya Iran na mataifa ya magharibi.