Serikali ya Nigeria yataka mazungumzo

Serikali ya Nigeria inatarajiwa kufanya mkutano na viongozi wa vyama vya kutetea wafanyikazi katika jaribio la hivi punde la kusitisha mgomo uliodumu wiki nzima kulalamikia hatua ya serikali kuondoa ruzuku kwenye bei ya mafuta.

Vyama hivyo tayari vimkatalia mbali pendekezo la serikali la kurejesha chini ya nusu ya ruzuku hiyo, ambayo kuondolewa kwake wiki mbili zilizopita kulipelekea bei ya mafuta kuongezeka maradufu.

Chama kikuu cha wafanyikazi wa sekta ya mafuta kimeonya kwamba kitaanza kuwaondoa wafanyikazi katika visima vya kuchimba mafuta iwapo makubaliano hayataafikiwa kufikia kesho jumapili.

Mgomo huyo tayari umegarimu uchumi wa Nigeria mabilioni ya dola kupitia ushuru uliopotea na kupelekea vifo vya watu katika makabiliano na maafisa wa polisi.