Aliyekuwa kiongozi Guatemala kushtakiwa

Aliyekuwa kiongozi wa kijeshi nchini Guatemala, Efrain Rios Montt, atashtakiwa kwa kuhusika katika mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya binadamu.

Jaji katika mahakama maalum iliyokuwa ikisikiliza kesi dhidi yake amesema kuwa kuna ushahidi wa kutosha wa kumshtaki na amemhukumu kifungo cha kutotoka nyumbani hadi kesi hiyo iaamuliwe.

Kiongozi huyo wa zamani alifikishwa katika mahakama kuu kusikiza tuhuma kadhaa dhidi yake. Mahakamani familia za waathirika wa mauaji hayo waliofika walimzomea kwa maneno makali.

Anatuhumiwa kutekeleza mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya binadamu, ikiwemo mauaji ya watu zaidi ya 1,770, ubakaji wa wanawake 1,500 na kuwatimua watu 29,000 kutoka makwao.