Uhasama watokota Sudan

Uhasama kati ya serikali ya Sudan Kusini na utawala wa Khartoum kwa mara nyingine umechochewa na mzozo kuhusu mafuta yanayopatikana katika maeneo ya mipaka ya nchi hizo mbili.

Uchumi wa mataifa haya mawili unategemea sana mapato yanayotokana na uuzaji wa mafauta hayo.

Uhasama huo pia umesababishwa na mzozo kuhusu mipaka na madai kuwa serikali hizo mbili hufadhili waasi ili kushambuliana.

Wachanganuzi wanasema kuwa mzozo huu ni njama ya kuyumbisha serikali ya Sudan Kusini.

Akiongea mjini London, mjumbe maalum wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, Hilde Johnson, ametoa wito kwa jamii ya kimataiafa kuingilia kati ili kusaidia mataifa hayo mawili kutatua mzozo huo na masuala mengine yaliyosalia kwa njia ya amani.

Hata hivyo mjumbe huyo amesema ni wazi kuwa Sudan Kusini inakabiliwa na matatizo mengi.

Miongoni mwao ni kukabiliana na athari za mashambulio yaliyotekelezwa na zaidi ya wapiganaji 1,000 dhidi ya kabila moja hasimu katika jimbo la Jonglei na kusababisha vifo vya mamia ya watu na maelfu ya wengine wakalazimika kuhama makwao.

Idadi kubwa ya wakaazi wa eneo hilo kwa sasa hawana mifugo ambao ni tegemeo lao maishani.