Wanajeshi wa Syria washambulia Homs

Kwa mara nyingine tena wanajeshi wa Syria wameshambulia mji wa Homs kwa mamia ya makombora katika maeneo ya makaazi kwa siku nzima.

Mwandishi wa BBC katika eneo la Homs amesema kuwa wakaazi wa eneo hilo wametaja shambulio la hivi sasa kama baya zaidi kuwahi kufanywa tangu maasi kuanza nchini humo zaidi ya mwaka mmoja uliopita.

Ripoti kutoka eneo hilo zinasema kuwa wanajeshi wa Serikali walilipua eneo linalotumiwa kama hospitali katika eneo hilo na kuwaua na kuwajeruhi raia kadhaa.

Mji wa Homs ndio umekuwa mstari wa mbele katika maasi ya kutaka kumtimua Rais Assad mamlakani. Serikali kwa upande wake imelaumu magaidi wenye silaha kwa mashambulizi hayo ya makombora.