Syria: wengi wauawa mji wa Homs

Vikundi vya upinzani nchini Syria vinasema kwamba majeshi ya serikali yameushaumbulia mji wa Homs kwa makombora mengi, licha ya rais wa nchi hiyo Bashar al-Assad kutoa ahadi ya kufanya mazungumzo na upinzani.

Mji huo wa Homs umekuwa ukishambuliwa kwa makombora kwa siku tano sasa; na majeshi ya serikali yanasemekana kukaribia maeneo yanayomilikiwa na vikundi vya upinzani.

Wanaharakati wanasema zaidi ya watu 40 wamefariki dunia kufuatia kurushwa kwa makombora lakini ni vigumu kubainisha jambo hili.

Mashambulio haya yanakuja siku moja baada ya Rais Bashar al-Assad kumhakikishia Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, huko Damascus kuwa mapigano yangesitishwa na mazungumzo kufanyika.

Urusi na China zilipiga kura ya turufu kupinga azimio la baraza la usalama la umoja wa mataifa wiki iliyopita.

Mwandishi wa BBC, Paul Wood, ambaye yuko nje ya mji wa Homs na wapiganaji waasi, anasema watu wa mji huo wanahofia mashambulio ya nchi kavu.