Ban Ki Moon aonya utawala wa Syria

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon, ametoa taarifa kali akionya kuwa mzozo wa kisiasa nchini Syria huenda ukasababisha maafa zaidi.

Bila kutaja mataifa yoyote, katibu huyo wa Umoja wa mataifa amesema uamuzi wa serikali za Urusi na Uchina kutumia kura zao za turufu kupinga vikwazo zaidi dhidi ya utawala wa Syria, umeifanya serikali ya nchi hiyo kuimarisha dhuluma dhidi ya raia wake.

Akiongea mjini New York, Bwana Ban amesema, ni jambo la kusikitisha kuwa mabalozi katika baraza la usalama la umoja huo walishindwa kuafikiana kuhusu mzozo huo wa Syria.

Amesema mateso ambayo raia wa Syria mjini wa Homs wamekumbana nayo ni ishara ya mambo mabaya zaidi ambayo huenda yakatokea siku zijazo.