Maldives: Rais wa zamani kukamatwa

Serikali ya Maldives imetoa hati ya kukamatwa kwa rais wa zamani wa nchi hiyo Mohammed Nasheed, na waziri wake wa zamani wa Ulinzi.

Maafisa kutoka chama cha Bwana Nasheed cha Maldivian Democratic wamesema hati hizo zilitolewa na mahakama ya uhalifu, lakini mkuu wa polisi mpya wa Maldives amesema hana habari ya kutolewa kwa hati hizo.

Bwana Nasheed anasemekana kuwa alilazimishwa kuondoka ofisini chini ya mtutu wa bunduki mapema wiki hii.

Jana, katika mji mkuu wa Maldives, Male, wafuasi wake walijeruhiwa wakati polisi walipojaribu kuzuia maandamano kupinga kung'olewa madarakani kwa rais Nasheed.