Obama ashtumu mauaji nchini Syria

Rais Obama ametaja mashambulizi ya makombora yanayoendelea kufanywa na wanajeshi wa Syria katika mji wa Homs kama mauaji ya kikatili. Alikariri wito wake kuwa Rais Bashar Al- Assad ang'atuke mamlakani.

Wakereketwa nchini humo wamesema kuwa watu 40 wameuawa katika siku ya sita ya mashambulio hayo kufuatia mashambulizi ya wanajeshi wa serikali.

Kulingana na wakereketwa hao, wilaya kadhaa zimeshambuliwa na vifaru, makombora na bunduki za kawaida.

Familia tatu ziliangamia baada ya kufukiwa katika vifusi vya nyumba zao zilizokuwa zimeshambuliwa.

Daktari mmoja katika hospitali ya muda mjini Homs amesema kuwa watu wengi wanaendelea kufariki katika hospitali kama hizo kwa sababu ya kukosa utunzi unaofaa.