Maandamano nchini Bahrain

Makabiliano yameendelea usiku kucha katika mji mkuu wa Bahrain, Manama huku nchi hiyo ikiadhimisha mwaka mmoja tangu kuanza kwa maandamano ya kudai demokrasia katika nchi za kiarabu.

Mkaazi mmoja wa eneo la Waislamu wa madhehebu ya Shia ameiambia BBC, kuwa maafisa wa usalama nchini Bahrain wametumia gesi ya kutoa machozi kutawanya waandamanaji.

Maelfu ya waandamanaji wanatarajiwa kujumuika katika kiunga cha Pearl katikati ya mji mkuu Manama, ambapo maandamano yalianza mwaka jana.

Idadi kubwa ya waandamanaji ni Washia walio wengi na wanataka demokrasia katika nchi hiyo yenye utawala wa kifalme unaoongozwa na Wasuni.