Murdoch yuko London kushughulikia mzozo

Tajiri wa vyombo vya habari duniani, Rupert Murdoch, amewasili mjini London kushughulikia mgogoro mpya unaokabili moja ya vyombo vyake vya habari.

Moja ya magazeti yake lenye mauzo makubwa nchini Uingereza, The Sun, limekumbwa na mgogoro, ambapo waandishi wake watano waandamizi, walihojiwa na polisi mwishoni mwa wiki, kwa tuhuma za kuwalipa polisi na maafisa wengine wa umma ili kupata habari wanazozihitaji kwa gazeti lao.

Wafanyakazi wa gazeti hilo wamekerwa na polisi kwa kutumia ushahidi uliowasilishwa na kamati iliyokuwa imeundwa kuchunguza ukiukaji wa maadili ya kazi baada ya kutokea kashfa ya udukuzi wa simu za mkononi, katika moja ya vyombo vya habari vya Bwana Murdoch, kulikosababisha kufungwa kwa gazeti maarufu la News of the World.