Wanajeshi wa NATO wauawa Afghanistan

Wanajeshi wawili wa shirika la NATO wamepigwa risasi na kuuawa katika siku ya tatu ya maandamano dhidi ya Marekani nchini Afghanistan. Maafisa wa Afghanistan wamesema wanajeshi hao walipigwa risasi na mwandamanaji aliyevalia sare za jeshi la Afghanistan.

Tukio hilo lilitokea wakati waandamanaji waliposhambulia kambi ya jeshi iliyoko mkoa wa Nangahar mashariki mwa nchi. Katika makabiliano hayo waandamanaji wawili pia waliuawa.

Kwingineko waandamanaji wanne wameuawa huku maandamano yakisambaa katika mikoa saba kaskazini mashariki mwa nchi.Raia hao wameghathabishwa na hatua ya kuteketezwa Koran kadhaa katika kambi moja ya jeshi la Marekani kitendo ambacho jeshi la NATO limesema hakikuwa cha makusudi.

Kundi la Taleban limetaka raia wa nchi za magharibi kulengwa kama kulipiza kisasi kitendo hicho.