Watu wa Syria wapata msaada

Afisa mkuu wa masawala ya kibinadamu katika umoja wa mataifa, Valerie Amos, yuko mjini Homs, Syria, ambako amefanya ziara fupi katika wilaya ya Baba Amr kitovu cha ghasia nchini humo.

Bi Amos aliambatana na wafanyakazi wa shirika la msalaba mwekundu ambalo hushirikana na shirika la kimataifa la Red Cross.

Msafara wa magari ya shirika hilo umekuwa ukisubiri tangu Ijumaa kuingia Baba Amr, iliyokuwa ngome ya upinzani, na ambayo ilishambuliwa na wanajeshi wa serikali kwa karibu mwezi mmoja.

Mamia ya watu walifariki kutokana na mashambulizi hayo. Mapema Bi Amos alikutana na waziri wa mambo ya nje wa Syria mjini Damascus, kuombea ruhusa wafanyikazi wa mashirika ya misaada kuingia katika eneo la Baba Amr.