Upinzani Syria wakataa mazungumzo.

Kundi kuu la upinzani nchini Syria limekataa ombi la mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa na Muungano wa nchi za Kiarabu, Koffi Annan kufanya mazungumzo na rais Bashar Al Assad, kama hatua ya kumaliza machafuko yanayoendelea nchini humo.

Burhan Ghalioun ambaye ni kiongozi wa baraza kuu la Syria ameelezea masikitiko yake akisema hawezi kujadiliana na rais Assad wakati akiendelea kuwaua raia wake.

Huku haya yakiarifiwa runinga ya Uturuki imesema majenerali wawili na Kanali wa kijeshi wameasi na kujiunga na upinzani.

Katika matukio ya awali ni wanajeshi wa ngazi za chini ambao wamekuwa wakiasi.

Aidha makundi ya wanaharakati yamesema majeshi ya serikali yameendelea kuyashambulia tena maeneo ya upinzani huko Homs.