Ugiriki yafutiwa baadhi ya madeni

Waziri wa fedha wa Ugiriki, Evangelos Venizelos amesema mchango wa sekta binafsi pamoja na wafadhili umesaidia kutatua tatizo la madeni linalokumba nchi hiyo.

Mpango huu unatoa hati dhamana za serikali kugharamia madeni ya nchi. Akitoa taarifa kwa bunge waziri huyo amesema chini ya mpango wa sasa zaidi ya Euro bilioni moja mkopo wa Uguriki zitafutwa ikiutaja kama hatua ya kihistoria. Awali serikali ilitangaza zaidi ya asili mia 85 ya wakopeshaji wa Ugiriki wameridhia kufuta baadhi ya deni.

Hii itawezesha serikali kutumia kipengele cha sheria kuwalazimisha wanaopinga kutolewa hati dhamana ili kugharamia madeni kuunga mkono mpango wa kutoa asili mia 95 ya hati dhamana hizo.

Mawaziri wa fedha kutoka kanda inayotumia sarafu ya Euro wanatarajiwa kukutana baadaye leo kutathmini mpango huo wa serikali ya Ugiriki.