"Okonjo-Iweala anatosha", Maafisa wa WB

Baadhi ya maafisa wa zamani katika Benki ya dunia wametoa taarifa ya pamoja ambapo wamemuunga mkono Waziri wa fedha wa Nigeria, Ngozi Okonjo-Iweala kuteuliwa Rais wa benki hiyo.

Kwa desturi Rais wa Benki ya Dunia huteuliwa mgombea anayependekezwa na Marekani wakati huu akiwa Jim Yong Kim.

Hata hivyo kwenye taarifa yao, maafisa hao 36 wa zamani wamesisitiza Kiongozi mpya ateuliwe kwa misingi ya ujuzi wake.

Kuna wagombea wengine watatu kwa wadhifa huo. Wagombea wote ni pamoja na bi.Okonjo-Iweala zamani akiwa mkurugenzi wa Benki ya Dunia, Waziri wa zamani wa fedha Colombia,Jose Antinio Ocampo pamoja na Jim Yong Kim, mtaalamu wa masuala ya afya na Rais wa chuo kikuu cha Dartmouth.

Mahojiano ya kumteuwa rais mpya kuchukua nafasi ya Robert Zoellick ambaye anatarajiwa kuondoka wadhifa wake ifikapo Aprili 20,yatafanyika wiki ijayo.

Taarifa ya maafisa hao wa zamani imesema bi Okonjo-Iweala ana ujuzi wa kutosha. Desturi ya kumteuwa rais wa Benki ya dunia huwa Marekani kushikilia nafasi hiyo nayo mataifa ya Ulaya yakishikilia uongozi katika Shirika la Fedha Duniani-IMF.