Vikwazo dhidi ya Burma kulegezwa

Maafisa wakuu wa Jumuiya ya Ulaya wameafikiana kimsingi kuondoa vikwazo vya kiuchumi walivyokuwa wamewekea taifa la Burma. Afisa mmoja kutoka Brussels amesema kuwa Mawaziri wa Kigeni walitazamiwa kuidhinisha mapatano hayo juma lijalo.

Hatua hiyo itawaondolea vikwazo vya safari maafisa wa Serikali hiyo ya Burma na kuliruhusu taifa hilo kuuza bidhaa zake katika mataifa wanachama wa Jumuiya ya Ulaya na pia kulihakikishia taifa hilo misaada ya maendeleo na uekezaji.

Hata hivyo vikwazo vya silaha havitaondolewa. Tayari Marekani na Australia wamelegeza vikwazo walivyowekea taifa hilo kufuatia marekebisho ya kisiasa ambapo uchaguzi umefanywa na kiongozi wa upinzani, Aung San Suu Kyi, amechaguliwa Bungeni.

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, aliunga mkono kulegeza vikwazo vya kiuchumi mwezi huuu, baada ya kuwa kiongozi wa kwanza kutoka mataifa ya Magharibi kutembelea Burma kufutilia mbali vikwazo hivyo vilivyowekwa.