Uchunguzi dhidi ya wanajeshi wasitishwa

Jeshi la Israel, limesitisha uchunguzi wake kuhusu vifo vya watu 21 kutoka familia moja nchini Palestina, ambavyo vinadaiwa kusababishwa na mashambulio ya anga yaliyotekelezwa na wanajeshi nchi hiyo mwaka wa 2009, katika ukanda wa Gaza.

Jeshi la nchi hiyo limesema hakuna mwanajeshi yeyote atakayefunguliwa mashtaka kuhusiana na tukio hilo na kukana madai kuwa kitendo hicho kilikuwa ni uhalifu wa kivita.

Aidha jeshi la Israel, limekana madai kuwa nyumba ambayo familia ya Samaouni, ilikuwa imetafuta hifadhi ililengwa makusudi.

Jamaa ya familia hiyo na wanaharakati wa kijamii nchini Israel, wamelaani uamuzi huo, na kusema kuwa jeshi haliwezi kujichunguza maovu yanayotendwa na baadhi ya maafisa wake.