Utafiti mpya kuhusu Saratani

Utafiti mpya umeonyesha kuwa kiasi kikubwa cha maambukizi ya ugonjwa wa saratani husababishwa na maradhi ambayo yanaweza kutibiwa au kuzuiwa kwa urahisi.

Utafiti huo unasema kuwa aina moja kati ya aina sita ya saratani kote duniani au maambukizi milioni mbili kila mwaka, husababishwa na maradhi hayo na kiasi hicho ni cha juu zaidi katika mataifa yanayostawi.

Kundi la wanasayansi waliofanya utafiti huo kutoka shirika la kimataifa la utafiti wa magonjwa ya Saratani nchini Ufaransa linasema kuwa saratani inapaswa kuchukuliwa kama maradhi yanayoambukizana.

Kundi hilo linasema juhudi zaidi zinastahili kufanywa kukabiliana na maambukizi yanayosababisha ugonjwa huo hatari kwa kutumia mbinu kama vile chanjo.