Watoto wa Afrika wanaasiliwa na wageni

Watetezi wa haki za watoto Barani Afrika wamesema idadi ya watoto wanaoasiliwa barani na raia wa kigeni imeongezeka katika miaka ya karibuni.

Shirika la kuteteta maslahi ya watoto ,The African Child Policy Forum limesema watoto wanaoasiliwa na walezi kutoka Marekani na nchi nyingine imeongezeka mara tatu katika kipindi cha miaka minane.

Ripoti ya shirika hilo imesema zaidi ya watoto 40,000 wametumwa nje ya nchi asilia katika kipindi hicho.

Hali ni tofauti kanda ya Amerika Kusini na Mashariki mwa Ulaya ambapo kuna udhibiti mkubwa wa watoto wanaoasiliwa na raia wa nje.

Mkurugenzi wa shirika hilo David Mugawe amesema kila mtoto ana haki ya kupata malezi bora na kujivunia utawamaduni wake katika mazingira yake asilia.