UN kuchunguza mauaji ya Syria

Afisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulika na masuala ya haki za binadamu imesema inachunguza mauaji ya halaiki yaliyofanyika katika mji wa Houla, Syria ambapo waathiriwa wengi wakiwemo watoto waliuawa hadharani.

Zaidi ya watu 100 waliuawa na wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wanasema ni wachache ambao waliangukia na makombora. Walioshuhudia wanasema wapiganaji wanaounga mkono serikali walitekeleza mauaji ya raia katika maeneo mawili.

Mjumbe wa kimataifa, Koffi Annan amekuwa akikutana na Rais wa Syria Bashar al Asaad mjini Damascus katika juhudi za kumshawishi kuridhia mpango wa amani. Bw. Annan ameonya serikali kwamba sharti ionyeshe nia ya kutatua mzozo wa nchi hiyo kwa njia ya amani.