Usafiri wakwama Jomo Kenyatta

Shughuli katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi, zimesitisha baada ya ndege moja inayomilikiwa na shirika la ndege la Misri kukwama katika eneo la kutua.

Kwa mujibu wa ripoti, ndege hiyo iliyokuwa ikiwasili katika uwanja huo mwendo wa sita za alfajiri, ikiwa na abiria 126 kutoka Cairo, ilikosa mwelekeo na kupita sehemu ya kutua inayoruhusiwa.

Kufuatia ajali hiyo ndogo, safari zote za ndege za kuingia na kutoka uwanja huo wa Jomo Kenyatta zimesimamishwa kwa muda.

Ndege zote zilizotarajiwa kutua katika uwanja huo zimeelekezwa kutua katika viwanja vya ndege vya Moi mjini Mombasa, Kilimanjaro nchini Tanzania na Entebe nchini Uganda.

Hakuna aliyejeruhiwa wakati wa tukio hilo.