Mubarak kupelekwa hospitali ya jeshi

Shirika la habari la serikali nchini Misri linasema maafisa huenda wakamuondoa rais wa zamani, Hosni Mubarak kutoka gerezani hadi kwenye hospitali ya kijeshi kwa sababu ya hali yake ya afya.

Bwana Mubarak tayari yuko katika hospitali ndani ya gereza baada ya kuhukumiwa kifungo cha maisha siku ya Jumamosi.

Alipatikana na hatia ya kuhusika kwa mauaji ya waandamanaji wakati wa maandamano yaliyomlazimisha yeye kuondoka madarakani. Muda mfupi baadaye, kukawa na taarifa kuwa hali ya afya ya Mubarak mwenye umri wa miaka themanini na nne imezorota.