Mshukiwa wa mauaji gesi akamatwa Japan

Polisi nchini Japan wamemkamata mtu wa mwisho aliyekuwa amejificha akituhumiwa kwa shambulio la gesi katika njia ya treni ya chini ya ardhi mwaka 1995 ambapo watu kumi na watatu waliuawa.

Vyombo vya habari nchini Japan vimesema mtuhumiwa huyo, Katsuya Takahashi, alikamatwa katika mgahawa mmoja jijini Tokyo.

Picha yake mpya ya siku za karibuni ilisambazwa katika vituo vya polisi nchini humo.

Alikuwa mmoja wa wanachama wa kikundi cha itikadi ya kidini cha Aum Shinrikyo, ambacho kilisambaza gesi ya sumu ya sarin katika mashambulio yaliyoratibiwa dhidi ya treni za chini ya ardhi.

Pamoja na watu waliouawa, watu elfu sita walijeruhiwa kwa gesi hiyo ya sumu inayoshambulia mishipa ya fahamu.

Wanachama wengine kumi na watatu wa kikundi hicho cha Aum Shinrikyo wanasubiri adhabu ya kunyongwa kufuatia mashambulio hayo nchini Japan.