China yaomba radhi kwa uavyaji mimba

Serikali ya Uchina imewaachisha kazi maafisa watatu na kuomba radhi kwa mwanamke aliyelazimishwa kutoa mimba ya miezi saba.

Picha ya mwanamke huyo, Feng Jianmei, na maiti ya kitoto chake ilichapishwa katika mtandao wa internet na kuvutia hisia kali kutoka kwa jamii ya kimataifa.

Mwandishi wa BBC anasema hatua hiyo kali imechukuliwa na Serikali kufuatia hisia zilizotolewa kwenye mtandao.

Maafisa wa Serikali katika jimbo la Shaanxi walimlazimisha aavye mimba hiyo kwa sababu hakuwa na fedha za kulipa faini kwa kosa la kumpata mtoto wa pili, ambalo ni kosa dhidi ya sera ya Uchina ya familia moja mtoto mmoja.