Sheria ya mapatano na waasi Colombia

Bunge la Colombia limepitisha sheria ya kuunda miongozo ya mazungumzo ya amani kati ya serikali na waasi.

Uamuzi huo wa bunge unaoungwa mkono na Rais Juan Manuel Santos, ni mwelekeo mpya kutoka sera za serikali zilizopita, ambazo zilikataa kujadiliana na waasi wa makundi ya FARC na ELN.

Muundo wa kisheria wa mazungumzo ya amani unatoa wito wa kutolewa adhabu ndogo kwa viongozi wa waasi iwapo watakiri makosa yao na kuwalipa fidia waathirika mara baada ya mazungumzo hayo ya amani.

Vikundi vya kutetea haki za binadamu na wanasiasa wa mrengo wa kulia wengi wao wakiwa karibu na rais aliyepita Alvaro Uribe wanasema hatua hiyo ya bunge itaruhusu makosa makubwa kufanyika bila ya kuadhibiwa.