Benki ya Barclays Uingereza kuchunguzwa

Serikali ya Uingereza imesema kuwa inaichunguza benki ya Barclays kwa makosa ya maadili katika utendaji kazi wake.

Benki hiyo pamoja na mashirika mengine makubwa ya fedha duniani yanachunguzwa na Vyombo vya usimamizi wa masuala ya fedha nchini Marekani, Ulaya na Asia. Baadhi ya taasisi kubwa za fedha duniani zinadaiwa zimekuwa zikifanya udanganyifu kuhusu viwango vya ukopeshanaji kati ya benki.

Benki za Citigroup, JP Morgan na Deutsche Bank ni miongoni mwa taasisi za kifedha zinazochunguzwa.

Jana, benki ya Barclyas ilipigwa faini ya dola milioni 452 kwa kudanganya kuhusu kiasi kinachoigharimu benki hiyo kukopa katika jaribio la kuongeza faida yake na kuonyesha kuwa benki hiyo ni salama kibiashara.