Watalii wa Israel washambuliwa Bulgeria

Watu watatu wamefariki na wengine wengi kujeruhiwa katika mlipuko wa bomu lililokuwa limetegwa ndani ya basi nchini Bulgeria.

Basi hilo lilikuwa limewabeba watalii wa Israel.

Maafisa wakuu nchini humo walithibitisha tukio hilo lilitokea katika mji wa Burgas ambako kuna uwanja wa ndege wa kimataifa.

Walioshuhudia tukio hilo, waliambia kituo cha televisheni cha Israel, kuwa waliona mtu mmoja akipanda basi hilo na punde tu mlipuko ukatokea

Polisi nchini humo, wanasema kuwa uwanja wa ndege wa Burgas kwa sasa umefungwa na ndege zote zilizokuwa zikielekea kaatika uwanja huo, kuamriwa kwenda kutua katika mji wa Varna.

Mwezi Januari kulikuwa na ripoti kuwa Israel ilikuwa imeomba Bulgeria kudhibiti usalama wake kwa watalii wa Israel wanaosafiri nchini humo kwa basi.