Mpinzani afariki nchini Cuba

Mmoja wa wapinzani wakubwa wa serikali nchini Cuba, Oswaldo Paya, amefariki dunia katika ajali ya barabarani katika jimbo la mashariki la Granma.

Mwanaharakati huyo wa haki za binadamu mwenye umri wa miaka sitini alikuwa akitaka yafanyike mabadiliko ya amani ya kidemokrasi nchini Cuba, na kutaka mjadala wa suala hilo uwahusishe wananchi wote wa Cuba.

Bwana Paya akapata umaarufu kimataifa alipokusanya sahihi zaidi ya elfu thelathini katika jaribio la kutaka kura ya maoni ifanyike kuhusu mabadiliko ya kidemokrasia nchini Cuba mwaka 2002.

Mwaka huo alipata nishani ya bunge la Ulaya ya haki za binadamu ijulikanayo kama Sakharov.