Iran yalaumu Marekani kwa mateka

Iran imesema kuwa imeweka usalama wa raia wake 48 mikononi mwa Marekani. Raia hao walitekwa nyara na kundi la waasi nchini Syria.

Naibu waziri wa mambo ya nje wa Iran , Hoseyn Amir-Abdo-llahian, ameilaumu Washington kwa kile alichokitaja kama kuunga mkono makundi ya waasi na kupeleka silaha nchini Syria.

Iran imesema mateka hao walikuwa katika ziara ya kuhiji nchini Syria ambapo walikuwa wakitembelea maeneo matakatifu ya Kishia.

Waasi wa Syria wanadai kuwa kundi hilo la mateka linajumuisha wafuasi wa kundi la majeshi ya Iran ambalo linaunga mkono majeshi ya Syria. Iran ni mshirika wa karibu wa utawala wa Rais Bashar Al Asaad.