Hisa za Standard Chartered zashuka

Bei ya hisa za benki ya Standard Chartered, nchini Uingereza, imeshuka sana baada ya wadhibiti wa maswala ya fedha nchini Marekani kuituhumu benki hiyo kwa kuficha zaidi ya dola bilioni 250 zilizotumika kwa biashara haramu na Iran.

Hisa za benki hiyo zilishuka kwa zaidi ya silimia 50 wakati wa ufunguzi wa biashara leo mjini London, baada ya hali sawa na hiyo kushuhudiwa Hong Kong.

Wadhibiti mjini New York, walisema kuwa benki hiyo ilighushi stakabadhi bandia kwa miaka mingi tu kusaidia Iran kuepuka sheria za nchi hiyo zinazoharamisha utengezaji wa pesa haramu.

Kwa mujibu wa wadhibiti hao, kitendo hicho kiliwanyima maafisa wa serikali ya Marekani fursa ya kupata habari muhimu na kuweka mfumo wa fedha wa Marekani wazi kwa tisho la kuvamiwa na makundi ya kigaidi.