Wavuvi watuhumiwa kuuawa Tanzania

Uongozi wa mkoa wa Geita nchini Tanzania umelazimika kuunda tume itakayofuatilia tuhuma za kuuawa kwa baadhi ya wavuvi katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa huo Magarula Said ,amesema taarifa za kuuawa kwa wavuvi hao zimemfikia baada ya kuandikiwa barua ya malalamiko ya mauaji hayo na Chama cha wananchi CUF.

Akizungumza na BBC Magarula amesema barua hiyo imetaja pia majina ya baadhi ya watu waliouawa. Amesema uongozi huo umezichukulia taarifa hizo kwa uzito na hivyo kuamua kuunda kamati ya watu wachache kulishughulikia mapema iwezekananvyo.

''Hatua tuliyoifikia kwa sasa ni kuunda kamati ya watu wachache ambayo tutawapa muda mfupi waweze kufanya kazi hiyo kwa kina ili tuweze kupata ukweli wa jambo lenyewe.'' Amesema.

Hata hivyo amesema idadi kamili ya watu waliouawa bado haijulikani hadi hapo ofisi yake itakapopokea majina kamili ya waliouawa kutoka kwa wanaoshughulikia jambo hilo.