Wanajeshi, Boko Haram wapambana Nigeria

Kulingana na wakaazi wa mji wa Maiduguri, kulikuwa na ufyatulianaji wa bunduki kwa masaa kadhaa kuanzia Jumapili asubuhi. Asubuhi hiyo maiti kadhaa zilionekana zikisafirishwa kwenye malori ya kijeshi.

Kanali victor Ebhaleme kutoka jeshi la Nigeria aliwambia waandishi wa habari kuwa wanachama wa kikosi maalumu walifyatuliwa risasi walipokaribia eneo la mkutano wa Boko Haram. Alisema wapiganaji 20 wa kundi hilo na mwanajeshi mmoja walifariki katika makabiliano hayo.

Kwa kawaida ni vigumu kuthibitisha habari kama hizi zinazohusisha wanajeshi wa Serikali wa wapiganaji wa Boko Haram.. Msemaji wa Boko Haram aliwambia waandishi wa habari kuwa hakuna hata mtu mmoja kati ya wanajeshi wao aliyepoteza maisha.

Alisema haingewezekana wapiganaji 20 wa Boko Haram kuwa mahali pamoja. Alieleza kuwa kuna uwezekano mkubwa kuwa waliouawa walikuwa raia wa kawaida.

Wachanganuzi wameanza kuuliza iwapo oparesheni za kijeshi zimeanza kufaulu katika kampeni za kuzima mashambulizi ya Boko Haram. Hata ingawa Serikali inadai kuwa inaendelea kufaulu katika kampeni zake lakini mashambulizi yaliyoanzia Kaskazini mwa nchi yameanza kusambaa hadi katikati mwa taifa hilo.

Kundi la kupigania haki za kibinadamu la Human Rights Watch linasema kuwa watu 1,400 wameuawa katika mashambulizi ya Boko Haram. Kundi hilo pia limeoorodhesha ukiukaji wa haki za kibinadamu uinaotekelezwa na wanajeshi wa Serikali.

Huku jeshi linapojitahidi kukabiliana na Boko Haram, limelaumiwa kwa kuwaua washukiwa kiholela na wakati huohuo kuwazuia watu bila kuwafikisha mahakamani. Tabia hizi, shirika hilo linasisitiza, linaaminiwa kuchochea uhasama zaidi kati ya watu hao.