Mkuu wa misaada wa UN awasili Syria

Imebadilishwa: 14 Agosti, 2012 - Saa 18:05 GMT

Mkuu wa misaada ya dharura ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Valerie Amos, amewasili nchini Syria huku wasiwasi ukiongezeka zaidi kuhusu raia wanaoathirika kutokana na mapigano kati ya vikosi vya rais Assad na wapinzani.

Ziara yake ya siku tatu itazingatia zaidi kuongezwa kwa misaada ya dharura kwa waathirika.

Mwandishi wa BBC anasema mapigano nchini Syria yameathiri kilimo na mavuno kwa mwaka huu na viwanda imebidi kufungwa

Raia milioni moja wamekimbia makazi yao, wakati watu laki moja na nusu wamekuwa wakimbizi katika nchi za jirani.

Msemaji wa shirika la chakula la umoja wa Mataifa-WFP, Elisabeth Byrs, amesema shirika hilo linakusudia kusaidia usambazaji wa misaada ya kibinadamu kwa watu wengi nchini Syria kadri inavyowezekana.

''Licha ya ugumu, shirika la mpango wa chakula limepanga kusambaza msaada kwa watu laki nane na nusu kufikia mwisho wa mwezi Agosti''. Amesema. ''WFP ina matumaini ya kuweza kuongeza misaada kwa watu wengi zaidi iwapo fedha zitawasili''. Ameongeza.

Elisabeth ameeleza kuwa lengo la shirika hilo ni kutoa msaada kufikia watu milioni moja katika wiki chache zijazo au kufikia mwishoni mwa mwezi Septemba.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.