Uingereza yarejesha msaada kwa Rwanda

Imebadilishwa: 6 Septemba, 2012 - Saa 08:44 GMT

Serikali ya Rwanda imekaribisha uamuzi wa Uingereza wa kuachilia fedha za misaada kwa Rwanda ambazo ilikuwa imezuia kutokana na shutuma kuwa Rwanda inasaidia waasi Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Waziri wa fedha wa Rwanda amesema kwamba uamuzi huo umetokana na mazungumzo yaliyofanyika baina ya Rwanda na Uingereza.

Serikali ya Uingereza itaanza tena kutoa msaada kwa Rwanda ikianza na nusu ya msaada huo ambao ulisitishwa miezi miwili iliyopita

Waziri wa Uingereza wa maendeleo ya kimataifa ,Andrew Mitchell, ametangaza kuchukua hatua hiyo baada ya kusema kuwa serikali hizo mbili zinafanya mazungumzo ya kutatua mgogoro huo ambao umesababisha zaidi ya watu laki mbili kupoteza makao yao tangu mwezi Aprili.

Rwanda imeelezea kuunga mkono mkutano wa kimataifa kuhusu eneo la maziwa makuu ambao unatafuta suluhu ya kudumu kwa mzozo unaokumba mashariki mwa Congo, kufuatia mzozo kati ya jeshi la serikali na kundi jipya la waasi la M23.

Kwa mujibu wa waziri Mitchell, Uingereza itatoa takriban dola milioni kumi na mbili ikiwa ni sehemu ya dola milioni 25 ambazo Uingereza ilisita kutoa kwa Rwanda.

Uingereza pamoja na wafadhili wengine wa kimataifa wakiwemo, Marekani, Sweden na serikali ya Udachi, zilisitisha msaada huo baada ya ripoti ya Umoja wa mataifa kutuhumu Rwanda kama mhusika katika uasi unaoendelea Mashariki mwa Congo.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.