Mapigano mazito yaripotiwa Syria

Imebadilishwa: 19 Septemba, 2012 - Saa 08:40 GMT

Pande zote zinazohusika katika vita nchini Syria zimeripoti kuwepo mapigano mazito na mashambulizi ya mabomu katika maeneo mengi hususan katika miji miwili mikuu Aleppo na Damascus.

Wanaharakati wanasema zaidi ya watu 150 wameuawa katika mapigano yaliyotokea hapo jana.

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, Amnesty International, limetoa ripoti likisema kuwa katika wiki za hivi karibuni vikosi vya serikali vimekuwa vikitumia silaha nzito na mashambulizi ya angani katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi na kusababisha maafa makubwa kwa raia.

Mojawapo ya maeneo yaliyolengwa katika mashambulizi ya hivi karibuni ni eneo la Kusini la Al Hajar Al Aswad. Pamekuwa na mapigano mengine mazito wakati vikosi vya serikali vikisemekana kulikaribia eneo hilo .

Wanaharakati wanasema hali kwa wakaazi katika eneo hilo ni ya kutamausha huku vikosi vikisogea kutoka pande zote na kulishambulia eneo hilo kwa milipuko.

Wanaharakati hao wametoa kanda za video wanazosema zinaonyesha helikopta zikiishambulia wilaya hiyo pamoja na kuonyesha zaidi ya miili 20 ya watu waliouawa katika eneo hilo.

Televisheni ya taifa ya Syria imesema wanajeshi wamewaua wanamgambo wengi katika eneo hilo ambao wamewataja kuwa magaidi. Pamekuwa na mapigano mapya pia katika mji mkubwa, Aleppo.

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu, Amnesty International, limetoa ripoti inayoeleza ongezeko la harakati za vikosi vya serikali katika eneo la Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo.

Amnesty imesema kuwa silaha nzito zinazotumika hazipaswi kutumiwa dhidi ya maeneo wanayoishi watu.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.