Waathiriwa waelezea tashwishi kuhusu ICC

Imebadilishwa: 26 Oktoba, 2012 - Saa 12:01 GMT

Waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2007/2008 wameelezea tashwishi kuhusu ushahidi uliokusanywa na mahakama hiyo dhidi ya washukiwa wanne wakuu wa ghasia za baada ya uchaguzi.

Washukiwa hao ni pamoja na Naibu waziri mkuu Uhuru Kenyatta, mbunge William Ruto, mwandishi wa habari Joshua Arap Sang, na aliyekuwa mkuu wa watumishi wa umma Francis Muthaura.

Wakiongea na mwendesha mkuu wa mashtaka ya ICC, Fatou Bensouda, waathiriwa wa mkasa wa moto katika kanisa la Kiambaa, mjini Eldoret, waliteta kuwa waathiriwa hawakuwahi kuhojiwa na tume maaruufu ya Waki pamoja na aliyekuwa mwendesha mkuu wa mashtaka Moreno Ocampo.

Tume ya Waki ndiyo ilipendekeza majina ya washukiwa wakuu wa ghasia za baada ya uchaguzi baada ya kukusanya ushahidi wake punde baada ya ghasia hizo.

Zaidi ya watu 40, wengi wao akina mama, wazee na watoto waliteketezwa moto katika kanisa hilo pembeni mwa mji wa Eldoret.

Bi Bensouda amewaambia waathiriwa hao kuwa ICC itafanya uchunguzi wa kina kuhakikisha kuwa waathiriwa na washukiwa wote wanapata haki.

Waathiriwa walilalamikia ukosefu wa habari zozote kuhusu kulipwa fidia kwa yaliyowakumba wakati wa ghasia hizo.

''Swala la fidia kwa waathiriwa linashughulikiwa na hazina ambayo ipo kwa sababu ya wathiriwa , sio mojawapo ya kazi za ofisi yangu.nitapeleka ujumbwe wetu katika mahakama kuwaambia kuwa shughuli hii inapswa kuwahusisha watu wengi iwezekanavyo.'' alisema Bi Bensouda

Bensouda atazuru kitovu kingine cha gasia hizo eneo la Burnt Forest. Bi Bensouda alisema kuwa upande wa mashtaka hautategemea ushahidi wa tume ya Waki pekee.

Wakenya wanne wameshtakiwa katika mahakama hiyo ya ICC kwa madai ya kuchochea ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.

Hapo Jana Bi Besouda aliwatembelea wathiriwa wengine katika maeneo ya Naivasha na Nakuru.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.