Mzozo umekwisha Zimbabwe - Zuma

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma amesema amesaidia kumaliza mvutano kati ya viongozi mahasimu wa Zimbabwe, baada ya kufanya ziara mjini Harare siku ya Ijumaa.

Image caption Mugabe na Tsvangirai

Bw Zuma amesema mzozo kati ya Rais Robert Mugabe na Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai umemalizika, baada ya saa nne za majadiliano.

Lakini wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaonya kuwa mazungumzo haya huenda yasilete matokeo ya mara moja.

Mzozo kati ya viongozi hao ni dalili ya kudorora zaidi kwa uhusiano kati ya mahasimu hao wa muda mrefu.

Image caption Jacob Zuma akiwa na Tsvangirai

"Wamekubaliana kuwa kulikuwa na matatizo ya mawasiliano kati yao, na tumetatua hilo, kwa hiyo wameamua kuendelea kukutana," amesema Rais Zuma.

Bw Zuma, Bw Mugabe na Bw Tsvangirai walionekana katika hali ya utulivu kwenye mkutano na waandishi wa habari, huku baadaye wakitabasamu na kupeana mikono.

Kiongozi huyo wa Afrika Kusini aliwasili siku moja baada ya Bw Tsvangirai kumpeleka mahakamani Bw Mugabe kuhusiana na uteuzi wa wakuu wa mikoa.

Image caption Zuma na Mugabe

Bw Tsvangirai amesema alitakiwa ashauriwe kwanza kabla ya uteuzi kufanyika, chini ya makubaliano ya kugawana madaraka, ambayo yalimpa uwaziri mkuu. Washirika wa Bw Mugabe wametupilia mbali madai hayo.

"Kwa ma mtazamo wangu, na kwa unyenyekevu, hii iko wazi kabisa. Chochote kitakachoamuliwa na Rais ni lazima na mimi nihusishwe kama Waziri Mkuu, lazima kwanza na mimi nikubali," amesema Bw Tsvangirai katika nyaraka za mahakamani, limeripoti shirika la habari la AFP.

Mwandishi wa BBC mjini Harare Brian Hungwe, amesema viongozi wote wawili wamekuwa wakizidi kuushutumiana juu ya kutofanikiwa kwa makubaliano ya kugawana madaraka, huku kila mmoja akitaka uchaguzi wa mapema ufanyike.

Mwezi uliopita Bw Mugabe alisema mkataba wa makubaliano ya serikali ya kugawana madaraka yasiongezwe muda, wakati muda wake utakapokwisha mwezi Februari.

Makubaliano ya kuuda serikali ya kugawana madaraka yalifikiwa baada ya uchumi wa Zimbabwe kuporomoka kufuatia uchaguzi uliozua utata mwaka 2008.

Image caption Robert Mugabe

Sehemu muhimu ya makubaliano hayo ilikuwa kuandika muswada wa katiba mpya.

Lakini mchakato wa kukubaliana kuhusu katiba mpya umesimamishwa kufuatia taarifa za mara kwa mara za kuwepo kwa ghasia za kisiasa.

Siku ya Alhamisi, Waziri wa Fedha Tendai Biti aliwaambia waandishi wa habari kuwa Zimbabwe ina fedha za kuandaa uchaguzi mwakani.

"Tumeandaa fedha za uchaguzi, na za kura ya maoni pia," Bw Biti aliwaambia waandishi wa habari baada ya kuwasilisha bajeti ya mwaka 2011.