Tatizo la watoto kukataa Dawa za ukimwi

Utafiti wa kwanza kufanywa kuhusu dawa ya kinga ya ukimwi miongoni mwa vijana wanaoishi na virusi vya ukimwi imeonyesha kuwa mwili wa mtoto 1 hadi 8 anaweza kuwa sugu dhidi ya dawa muhimu zilizotengenezwa kwa ajili ya kupunguza makali ya virusi vya ukimwi.

Utafiti huo ulichunguza hali za watoto 1000 kote barani Ulaya. Wataalamu wanasema kuwa mojapo ya matatizo nyeti ni ladha ya dawa, ambayo inaweza kuwachukiza wagonjwa na kukwepa kuitumia kama wanavyohitajika kufanya.

Tiba kuu ya ukimwi ni dawa ijulikanayo kama antiretroviral. Mchanganyiko wa dawa hizi hutumika kwa kupunguza kiwango cha makali ya virusi vya ukimwi mwilini. Hilo husaidia kwa kumpunguzia mgonjwa hali ya kudhoofika na kumsaidia kupata nafuu ya athari nyingine zinazosababishwa na ukimwi.

Kwa utafiti huu pekee Madaktari wa Baraza la utafiti wa matibabu nchini Uingereza walichunguza watoto kutoka nchi nane za Ulaya ikiwemo Uhispania,Ireland na Uholanzi.

Utafiti wao uligundua kwamba 1 kati ya watoto 8 alikuza kikwazo cha mwilini dhidi ya dawa aina tatu zilizopo kwa ajili ya vijana, waliotumia dawa hizo kwa kipindi cha miaka mitano idadi kubwa kuliko miongoni mwa watu wazima.

Utafiti huu unazua masuali juu ya ubora wa dawa hizi kwa watoto hao wanaoishi na virusi na ukimwi. Virusi vinaweza kuwa sugu kwa dawa ikiwa mgonjwa hatotumia dawa kwa kila siku - mara nyingi kwa siku kwa maisha yake yote.

Wataalamu wanaoendesha utafiti huu wanadokeza kuwa ni kazi kubwa kuwashawishi watoto na wavulana kuendeleza tabia ya kutumia dawa zenye ladhaa inayochukiza.

Kutokana na utafiti huo wataalamu hawa wameyataka makampuni yanayotengeneza dawa pamoja na wachunguzi wa ubora wa dawa wajitahidi kutengeneza dawa nyembamba, rahisi kutumia bila ya kuwa na ladhaa ya kuchukiza. Wanahisi kuwa hili huenda likasaidia kunusuru maisha ya watoto milioni 2 wanaoishi na maradhi ya ukimwi kote duniani.