Syria: Urusi kuruhusu misaada kuingia Aleppo

Chanzo cha picha, Reuters
Misaada ya kibinadamu inahitajika sana mjini Aleppo, Umoja wa mataifa umesema
Vikosi vya Urusi vinakaribia kusitisha kwa muda harakati za kijeshi katika mji wa kaskazini mwa Syria wa Aleppo kuruhusu kuingizwa kwa misaada ya kibinadamu inayohitajika sana. Haijawa wazi ikiwa makundi ya waasi wa Syria pia yatasitisha mapigano katika muda uliokubaliwa wa saa tatu.
Lakini maafisa wa Umoja wa Mataifa wanasema muda huo ni mfupi sana na hautoshi kusaidia idadi kubwa ya watu wanaohitaji msaada .
Mapigano makali yamekua yakiendelea mjini Alepo baina ya waasi na vikosi vya Syria vinavyoungwa mkono na Urusi.
Kuna pia ripoti za mashambulio ya gesi ya sumu katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi. Wahudumu wa matibabu wanasema kuwa watu wanne wamekufa na wengine wengi wamejeruhiwa. Gesi hiyo inadhaniwa kuwa ni ya aina chlorine iliyoangushwa katika bomu la pipa.
Chanzo cha picha, AFP
Umoja wa Mataifa unasema mashambulio yanayolenga hospitali na kliniki hayajakoma
Awali daktari aliebaki katika eneo linaloshikiliwa na waasi mashariki mwa mji wa Allepo alimuomba rais wa Marekani Barack Obama aingilie kati awasaidie raia 250,000 walioko huko.
Barua hiyo ilimtaka Obama kuweka marufuku ya kusafiri kwa ndege kwenye anga la Aleppo ili kuzuia mashambulio ya ndege.
Harakati zote za kijeshi za Urusi, mashambulio ya makombora ya anga yatasitishwa baina ya saa nne na saa saba, alieleza afisa wa wizara ya ulinzi alipokua akitoa maelezo mjini Moscow siku ya Jumatano.
Chanzo cha picha, AP
Urusi inapendekeza kutoa muda wa saa tatu wa kusitisha mashambulio ya makombora ya anga
Laiki mratibu wa shughuli za misaada ya dharura wa Umoja wa Mataifa Stephen O'Brien amesema kuwa kukidhi mahitaji ''unahitaji bara bara mbili na unahitaji saa 48 kuwezesha malori ya misaada kuingia."
"Mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa na washirika wake wako tayari kuwasaidia raia kote mjini Aleppo. Misaada iko tayari kwa kuanza kusambazwa (mgao wa chakula), madawa, magari ya kubebea wagonja,mafuta kwa ajili ya genereta , maji na misaada mingne Zaidi.
"Tutaendelea kutumia njia zote zilizopo na mbinu za kufanya hili, ile ya kupitia mpakani mwa Uturuki. Tunaweza kusambaza misaada katika muda wa saa 24 hadi 48, kama tunaweza kuwafikia walengwa kwa usalama," alisema Bw O'Brien.
Mapigano yamechacha mjini Aleppo siku za hivi karibuni, huku waasi wakifunga njia kuu za serikali magharibi mwa mji huo.