Maelfu ya wahamiaji waokolewa katika pwani ya Libya

Vikosi vya uokoaji vya majini vya Italy vimesema vimeratibu uokoaji wa wahamiaji elfu sita na mia tano katika bahari ya Mediterania siku ya jumatatu. Kwa mujibu wa vikosi hivyo, hii ni oparesheni kubwa zaidi kuwahi kutokea katika miaka ya hivi karibuni.

Taarifa za oparesheni hiyo ambayo ilihusisha vikosi kutoka nchi mbalimbali zilitolewa katika mtandao wa Twitter, na imeelezwa kuwa ni moja kati ya oparesheni kubwa ya uokoaji kuwahi kutokea kwa miaka mingi.

Katika moja ya oparesheni hizo, raia kutoka Eritrea na Somalia wameonekana wakiruka baharini huku wakikimbilia vikosi vya uokoaji.

Maelfu ya raia wa kiafrika, wengi wao wakitafuta maisha bora barani ulaya, mara nyingi husafirishwa katika madau ambayo hayana hadhi ya kuhimili mikiki mikiki ya bahari.

Image caption Mmoja wa wahamiaji akimbeba mtoto wake wa siku tano kuelekea katika boti ya waokoaji

Katika msafara huo pia, kuna wakimbizi kutoka maeneo ya vita kama mashariki ya kati na Afghanistan. Wengi wao wamepoteza maisha yao.