Mashabiki wamtetea Chris Brown

Chris Brown
Image caption Chris Brown

Mashabiki wanamtetea mwanamuziki Chris Brown ambaye anakabiliwa na shtaka la kushambulia baada ya kumtishia kwa bunduki mwanamke mmoja katika nyumba yake.

Wakili wake anadai kwamba madai hayo ni ya uongo na mashabiki wamekongomana katika mitandao ya kijamii kumuunga mkono.

Hii sio mara ya kwanza kwa Brown kukabiliwa na sheria ikiwemo visa kadhaa vya ghasia alivyotekeleza hapo awali.

Lakini ni kwa nini mashabiki wengi wanampenda?

Image caption Mashabiki wanaomtetea Chris Brown

Chris Brown alimshambulia aliyekuwa mpenziwe Rihanna mwaka 2009 ambapo ilikuwa habari kuu ya mwaka.

Maelezo ya shambulio hilo katika ripoti ya polisi pamoja na picha za majeraha ya Rihanna zilifichuliwa katika vyombo vya habari na kusababisha hisia kali.

Polisi waliitwa makazi ya Chris Brown na mwanamke aliyeomba msaada saa tisa usiku wa kuamkia leo.

Malkia wa urembo, Baylee Curran ameambia gazeti la LA Times, kwamba mwanamuziki huyo alimwelekezea mtutu wa bunduki.

Hata hivyo walizuiwa kuingia na ilibidi wasubiri hadi kupata idhini ya jaji kabla kufanya msako wa kutafuta bunduki katika makaazi hayo.

Mwanamke huyo aliyewaita polisi baadaye aliambia vyombo vya habari kwamba walitofautiana na Brown kuhusu majohari.

Alisema alikuwa ameingia kwa Bw Brown akiwa na rafiki yake na mshirika wa kibiashara na alikuwa akiangalia mkufu wa thamani uliokuwa umevaliwa na mwanamume mmoja pale mwanamuziki huyo alipomkaripia na kumtaka aondoke mara moja akiwa amemwelekezea bunduki.