Askofu wa kanisa la England ametangaza wazi kuwa anashiriki mapenzi ya jinsia moja

Askofu Nicholas Chamberlain
Image caption Askofu Nicholas Chamberlain, amesema kuwa walioshiriki katika mchakato wa kumteua mwaka uliopita walialewa fika mwelekeo wake wa jinsia.

Askofu mmoja wa kanisa la kianglikana nchini Uingereza amekuwa wa kwanza kutangaza hadharani kuwa anashiriki mapenzi ya jinsia moja na sasa yuko kwenye uhusiano.

Kasisi Nicholas Chamberlain, amesema kuwa walioshiriki katika mchakato wa kumteua mwaka uliopita walialewa fika mwelekeo wake wa jinsia.

''Watu wanajua nashiriki mapenzi ya jinsia moja, lakini si kitu cha kwanza nachoweza kumwambia yeyote. Jinsia ni sehemu ya yule niliye, lakini ni kazi yangu ya kitume ambayo ninataka kuiangazia ."

Nicholas Chamberlain anasema hata hivyo anafuata kanuni za kanisa zinazosema kuwa haruhusiwi kuoa.

Msemaji wa kanisa la England amesema: "Nicholas hajamkera yeyote na amekua wazi na mkweli ukiuliza. Suala lake si la siri, ingawa ni la kibinafsi kama ilivyo kwa wale walio katika mahusiano ya kimapenzi ."

Inadhaniwa kuwa hakuna askofu yeyote anayehudumu aliyewahi kutangaza hadharani msimamo wake wa kingono.

Kanisa la kianglikana kote duniani limegawanyika sana miaka ya hivi karibuni kuhusu masuala yanayohusu mwelekeo wa kijinsia na kutawazwa kwa makasisi walio katika mapenzi ya jinsia moja.