Wafanyakazi 25,000 wa serikali kufutwa Zimbabwe kupunguza gharama

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Waziri Patrick Chinamasa amewaambia wabunge kuwa ni wakati wa 'kufunga mikanda'

Waziri wa fedha wa Zimbabwe ametangaza kwamba serikali itafuta ajira 25,000 katika sekta ya huduma za raia kwasababu haiwezi kumudu gharama,limeripoti gazeti linalomilikiwa na serikali.

Patrick Chinamasa ameliambia bunge kwamba mishahara na marupurupu pia vitakatwa na hakutakuwa na malipo ya tunuku kwa muda wa miaka miwili.

Wengi miongozi mwa wafanyakazi wa umma hupokea pesa za marupurupu nyakati za Christmas, maarufu nchini humo kama "hundi ya tarehe".

Mabalozi wa Zimbabwe katika nchi za kigeni pia wataathiriwa na idadi ya balozi na balozi ndogo za zimbabwe itapunguzwa .

Zimbabwe inakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa fedha kwa sasa: Wafanyakazi wa umma wamekuwa wakichelewa kupata mishahara yao ya kila mwezi, ikiwa ni pamoja na polisi pamoja na wanajeshi.

Hii ni kwasababu nchi haikusanyi kodi ya kutosha ya kuwalipa.

Gazeti la Herald linasema kwamba kiwango cha mishahara ya taifa hilo inategemea 97% ya ushuru.

Hatua hiyo iliyotangazwa na Bw Chinamasa inatarajiwa kupunguza gharama za ajira hadi 60%, limesema gazeti hilo.

Hali mbaya ya uchumi nchini Zimbabwe imesababisha maandamano makubwa ya upinzani dhidi ya serikali katika kipindi cha miezi michache.