Amnesty International yawagusa polisi wa Nigeria

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari

Shirika la Haki za Binadamu la Amnesty International limetoa ripoti, likilaumu Polisi nchini Nigeria kwa utesaji, ukatili na rushwa.

Ripoti hiyo iliyochapishwa leo inadai kwamba, Kitengo maalumu cha Polisi nchini humo kilichoandaliwa kwa ajili ya kupambana na uhalifu, kimekuwa kikitesa watu waliowaweka kizuizini.

Ripoti hiyo inasema kuwa wanafanya hivyo kwa ajili ya kuwatisha kuweza kukiri kosa na kuwafanya waweze kutoa rushwa.

Kwa mujibu wa Amnesty International, Kitengo hicho cha polisi, kinachojulikana kama kikosi maalum cha kupambana na Uhalifu kinaogopwa sana nchini Nigeria, kutokana na ukatili wake.

Wanaharakati wa masuala ya haki za binadamu wanasema wamepata ushuhuda kutoka kwa watu waliowahi kushikiliwa juu ya jinsi njia za mateso ya kutisha zilivyotumika, ikiwemo kunyongwa, kuachwa na njaa, kupigwa risasi na vitisho vingine huku wakishikiliwa na polisi wala rushwa.

Ripoti hiyo imeeleza pia kikosi hicho maalum cha polisi kimeandaliwa kwa ajili ya kuwalinda watu badala yake kimekuwa kikiwajengea watu hofu na mazingira ya rushwa.

Amnesty Inertaional pia imesema polisi wamekuwa wakivunja haki za binadamu kwa kuwakamata watu, kuwatesa mpaka ''watakapo kiri'' ama kuwapa rushwa maafisa ili waachiwe.

Huwashikilia watuhumiwa hao katika vizuizi tofauti kikiwemo cha Abuja kinachojulikana kama machinjio, ambacho kwa mujibu wa Shirika la Amnesty International kinawashukiwa 130, ikiwa ni watu wengi, zaidi ya uwezo wa jengo hilo.

Hata hivyo Polisi nchini Nigeria bado hawajaijibu ripoti hiyo.