IS limeifyetulia kambi ya jeshi la Marekani kombora la kemikali Iraq

Operesheni ya kujaribu kuudhibiti upya mji wa Mosul inatarajiwa katika wiki zijazo Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Operesheni ya kujaribu kuudhibiti upya mji wa Mosul inatarajiwa katika wiki zijazo

Kombora lililofyatuliwa na wanamgambo wa Islamic State dhidi ya kambi ya jeshi la Marekani nchini Iraq lilikuwa na kemikali, jeshi la Marekani limethibitisha.

Hakuna aliyejeruhiwa katika shambulio hilo la Jumanne katika kambi ya jeshi ya Qayyarah karibu na ngome ya IS Mosul.

Jenerali wa jeshi la maji Joseph Dunford, mwenyekiti wa vikosi vya pamoja vya Marekani, amesema uwezo wa kundi hilo kuwasilisha silaha za kemikali ni mdogo sana.

Lakini shambulio hilo, ameongeza, ''linatia wasiwasi".

IS kwa muda mrefu limetuhumiwa kutengeneza na kutumia silaha za kemikali nchini Iraq na Syria, ambako pia linadhibiti maeneo.

Jenerali Dunford ameiambia kamati ya huduma za jeshi katika bunge la Senati Marekani Alhamisi kuwa kombora hilo ilikuwa na kemikali aina ya "sulphur-mustard blister agent".

Katika kiwango cha kutosha, kemikali hiyo inaweza kuwaua watu kwa kuchoma ngozi, macho na njia ya mtu kupumua.

Mosul, mji wa pili kwa ukubwa Iraq, umedhibitiwa na IS kwa miaka miwili iliopita na mapambano ya kuudhiibiti upya yanatarajiwa kuanza katika wiki zinazokuja.

Vikosi vya Marekani vinatoa usaidizi kwa vikosi nchini humo wakati vinapojitayarisha kwa operesheni hiyo.