MONUSCO kutumwa Kinshasa wakati wasiwasi wa kisiasa unaongezeka

MONUSCO Haki miliki ya picha AFP

Umoja wa mataifa unawaondoa mamia ya walinda amani wake kutoka mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo hadi Kinshasa kusaidia kukabiliana na uwezekano wa ghasia kufuatia kuahirishwa kwa uchaguzi wa urais, AFP limewanukuu maafisa wa Umoja huo.

Takriban wanajeshi 300 na polisi kutoka kikosi cha MONUSCO watakuwa Kinshasa, eneo ambako ghasia zilisababisha vifo vya watu kiasi ya 49 mwezi uliopita, maafisa wanasema.

"Tunapanga kwa hali yoyote na tumechukua hatua kuimarisha uwepo wetu Kinshasa," mkuu wa kikosi cha amani Herve Ladsous amesema.

Hatahivyo, huenda wanajeshi hao wanaotumwa wasitoshe iwapo mji mkuu huo utashuhudia ghasia kwa ukubwa, ameonya.

"ni muhimu tukumbuke kuwa Kinshasa ni mji wa takriban watu milioni 11 na MONUSCO haina idadi ya kutosha ya wanajeshi na pia jukumu la kutoa usalama," amesema.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mamia ya watu walijitokeza mwezi uliopita katika maandamano ya kumpinga rais Kabila

Wasiwasi wa kisiasa umeongezeka katika kinachoonekana kuwa jitihada za rais Kabila kusalia madarakani.

Makubaliano yamefikiwa wiki hii kusukuma mbele uchaguzi wa urais hadi Aprili 2018.

Lakini upinzani umesusia makubaliano hayo na umeitisha maandamano makubwa Jumatano.

Huwezi kusikiliza tena
'Kadi ya njano' kwa rais Kabila

Mjumbe wa Umoja wa mataifa kwa Congo, Maman Sambo Sidikou, wiki iliopita ameonya kuwa huenda nchi hiyo ukaingia katika hatari ya kukumbwa na ghasia iwapo hakuna jambo litakalofanyika kukabiliana na mzozo huo.