Huduma kama ya Uber kwa wakulima India kukodi matrekta

Mkulima India Haki miliki ya picha Thinkstock

Huduma mpya ya simu iliyoundwa kwa mfano wa Uber - huduma ya teksi, imezinduliwa India.

Imenuiwa kufanya kuwa rahisi kwa wakulima kukodisha ma trekta.

Wakulima wadogo hawana uwezo wa kununua matrekta yao binafsi na mara nyingi hulazimika kukodi kwa bei ghali.

Sasa kampuni ya kutengeneza magari Mahindra and Mahindra imezindua app ya simu ijulikanayao kama Trringo inayotoa huduma ya kukodi kwa saa trakta kwa kiasi ya kati ya rupi 400 na 700 ($6).

Huduma hiyo pia itapatikana kwa kupiga simu- iliyo muhimu kwasababu maeneo mengi ya mashinani India hayana huduma ya intaneti.

Huduma hiyo imeanzishwa katika jimbo la Karnataka kufikia sasa na inatarajiwa hivi karibuni kusambazwa kwingine ikiwemo majimbo ya Gujarat, Madhya Pradesh na Maharashtra.

Matrakta na madereva wake watatumwa kwa wakulima kupitia vituo 20 kote Karnataka.

Akizungumza kuhusu huduma hiyo kwa gazeti la New York Times, afisa mkuu mtendaji Rajesh Jejurikar amesema mpango uliopo wa kukodi 'unamlemea mkulima', akiongeza kuwa wengi wanahisi ni kama 'wanaomba'.

Kampuni hiyo inafikiria iwapo kuanzisha huduma ya kukodisha mashine nyengine za ukulima katika huduma kama hiyo.