Burundi yazima makundi ya kutetea haki za binadamu

Raia nchini Burundi wakiandamana barabarani, Bujumbura
Image caption Raia nchini Burundi wakiandamana barabarani, Bujumbura

Burundi imepiga marufuku makundi 10 ya kutetea haki za binadamu, huku muungano wa kutetea haki na maslahi ya waandishi habari pia, ukivunjwa.

Hiyo ni hatua ya hivi punde zaidi ya kupambana na ghasia.

Mashirika matano yamevunjwa kabisa, likiwemo lile la Protection of Human Rights and Detained Persons (APRODH), Wizara ya ndani imesema.

Shirika hilo lilikuwa likiongozwa na mwanaharakati Pierre Claver Mbonimpa, aliyehamia bara Ulaya mwaka jana baada ya kunusurika jaribio la kumuuwa, iliyotekelezwa na watu waliokuwa na silaha wasiojulikana katika mji mkuu Bujumbura.

Image caption Pierre Claver Mbonimpa, mtetezi wa haki za binadamu

Aidha wizara hiyo inaongeza kusema kuwa, mashirika mengine matano zaidi likiwemo Iteka, SOS-Torture and Burundian Union of Journalists, yamesimamishwa tu kwa muda.

Kwa mjibu wa taarifa ya shirika la habari la Reuters, Wizara ya maswala ya ndani ya taifa, inayalaumu mashirika hayo 10 "kwa kuonyesha chuki" nchini Burundi na "kutatiza utulivu wa umma na usalama wa taifa".

Burundi imekumbwa na ukosefu wa usalama tangu Rais Pierre Nkurunziza alipotangaza mwezi April mwaka 2014, kuwa atakawania tena kiti cha Urais kwa muhula wa tatu.

Hatrua hiyo ilisababisha ghasia kubwa huku majemedari wake jeshini wakipanga jaribio la mapinduzi, lakini likatibuka.